Zangu zifike salamu, nangoja yako jawabu
Bado niko mumu humu, kaniachia taabu
Najikaza nasaumu, rudi naomba jaribu
Niambie utakamu, gonjwa hili ulitibu
Hukunipa mi ilani, hata ya mwisho kwaheri
Ulienda pande gani, pekee ulisafiri
Naikosoa imani, kidogo niwe kafiri
Hakuna wa kunihani, kapona wanafikiri
Lala salama msena, ujumbe utaupata
Najua tutakutana, namna naitafuta
Wa kunipa dira sina, Jalali atamleta
Yabaki kuwa ya jana, maisha mwendo twapita