We mnyang'anyi jameni, sasa mbona hivi kweli
Nasema nawe mhuni, waona hii halali?
Nimechumia juani, usiku pia silali
Sasa hapo kivulini, wakula ya kwangu mali
Wazunguka na kiburi, kwangu chungu na machozi.
Mjini sasa ni pori, hayawani we jambazi
Yanizidi sana mori, wanizidia ujuzi
Nitajua yako siri, wizi nayo sio kazi
Itawa telezi miti, njia tu zitafungika
Utafikia tamati, itawa finyu mipaka
Kuishi nayo bahati, yako nayo tutapoka
Ukipoteza sijuti, kulaani sitachoka