Tamu imekuwa chungu, raha geuka karaha
Nalilia nchi yangu, yadhorora yake siha
Kenya kipenzi chungu, nafata gani nasaha
Lavunjika hili jungu, tunaipoteza njia
Kosa gani tunatenda, vijana kujieleza
Raisi tunakupenda, sauti tutazipaza
Kenya itabaki nyonda, sababuyo kujijaza
Mlima unaupanda, tutazidi kujikaza
Mama mboga analia, bodaboda sasa bubu
Upole twajifilia, yatuzidi masaibu
Wapi pa kukimbilia, serikali tupe jibu
Tueleze yenu nia, wacheni kutusulubu
Hatutachoka vijana, wembe nao ule ule
Tarudi tena na tena, sikiza zetu kelele
Kesho itazidi jana, hili ni sugu upele
Mshafika kwenye kona, imani ipo miale