Penzi Kibarua

by JackSwaleh , August 7, 2024

Nakukosea kwa kweli, nimekosa kutimiza
Ni ile ile tu hali, ya kesho yabaki giza
Sijui cha kubadili, nashinda nikikuwaza
Naanza kujikubali, kuwa nawe sitaweza

Ajira nimeshikika, bosi hatuelewani
Muda hata wa kupoka, naukosa ratibani
Yaja siku itafika, zidi kuwa na imani
Sitakupa uhakika, kuja kukuona lini

Usiteme penzi letu, jikaze lazizi wangu
Hisia zisiwe butu, nijifie kwa machungu
Itaja kuwa sawa tu, atatuwezesha Mungu
Hatuachi peke yetu, litapotea ukungu

Unaeza penda kusoma: "Uanadamu Adimu"