Niwacheni tu jamani, hamuwezi nielewa
Zimezidi zenu shani, semi zenu zaniwawa
Mwang'ata kama kunguni, mwaumiza kama chawa
Haya yangu madhumuni, najua sijachelewa
Mzaha sasa usaha, mie munanihujumu
Raha sasa karaha, kamwe munanidhulumu
Mashehe hadi kwa sheha, sio abu hadi mamu
Mwanitoa hadi siha, tulieni anakamu
Ninaye yu faraghani, sipendi kubaramaki
Siku yaja subirini, musinitie hamaki
Kaskazini kusini, magharibi mashariki
Ninaye wa kwangu hani, dira nilishaipiki