Nilipotoka ni Mbali

by JackSwaleh , August 15, 2024

Nilipotoka ni mbali, kesho nayo majaliwa
Namshukuru Jalali, maisha kanipa mbawa
Kanilinda zote hali, kwangu tamu tu mliwa
Hapa ni kwangu manzili, mie nimebarikiwa

Raha ninayo moyoni, fikira nazo tulivu
Wa pili shajua nani, kapata wangu ubavu
Napata yangu mapeni, tazidisha zangu nguvu
Ninayo sasa ramani, maarifa yamevuvu

Dunia tutaondoka, hebu raha jipe wewe
Siku nazo zapunguka, fungua ya kwako ndewe
Milango itafunguka, ufurahi pia nawe
Mawaidha haya daka, wa kusahau usiwe

Unaeza penda kusoma: "Naamini Nitafika"