Ndoa jamani ndoano, mwanamwali sikimbie
Nimeshaona watano, si usemi msikie
Kuigaiga mifano, mbio mbovu mtulie
Mambo mazuri rafiki, upesi si mwendo wake
Ndoa jamani ndoano, ilo na chambo pembeni
Yavutia kwa maono, ushoboke masikini
Mvuvi ja konokono, katu hayumo mbioni
Subira yake mvuvi, au mbio ya samaki?
Ukishaimeza chambo, ndio Mwanzo wayo ngoma
Bado kidogo kitambo, mwanga uanze zizima
Ukisitajabu mambo, janga umeshalichuma
Majuto ni mjukuu, nayo hukuja kinyume
Ni vema kusitasita, usikize kwa makini
Kwenye mema kujikita, mwema upate baini
Wa tabia za kunata, mlandane kwa undani
Safari ya mafanikio, taratibu ndio mwendo
Mie kikembe wa mama, sina mengi duniani
Ninanena kwa hekima, ya yule wangu mwandani
Alitangulia zama, amelala kwa amani
Somo na ni babu yangu, Ngangah Kizito Efumbi