Mpungufu binadamu, yeyote kiasi chake
Kuwa kamili adimu, kila mja na makeke
Yeyote yamugharimu, kuficha ubaya wake
Ni hujuma kulaumu, ati sema ikutoke
Kunena siwe mwepesi, legeza za kwako ndewe
Waelewe adinasi, usipo waache wawe
Wajali wanavyohisi, chunga mori usilewe
Maisha mwendo kasi, upole usilemewe
Twapita tu duniani, usipoteze wakati
Jitilie maanani, wachana na umati
Hamuna lolote geni, wachana nazo kamati
Hata kwa zao ilani, heshimayo masharti