Moyo wangu wasumbuka, yaganda ya kwangu damu
Nafsi yasononeka, hali kwani yahujumu
Mwenzenu nadhoofika, maisha yanidhulumu
Hadi lini kufinyika, tayari nishagharimu
Adimu hizi mihela, majukumu yazidia
Hamuna hata cha kula, mate yanikaukia
Uko wapi ewe Mola, mwanao na jifilia
Naziwacha hadi sala, sina pa kukimbilia
Sitachoka kujituma, bidii nitaongeza
Mabonde nayo milima, naamini nitaweza
Hatua nitazipima, jasho nalo kupanguza
Alivyonifunza mama, upole nitajikaza