Mjini kimeumana, nazidiwa maarifa
Mazito yananibana, zinaongezeka nyufa
Najaribu kukazana, marefu sana masafa
Ndoto zabakia dhana, mkweche nango ja mafa
Maisha huku magumu, heri kule kijijini
Najificha mumu humu, nazidiwa na madeni
Matatizo yanichumu, sijiwezi sibishani
Upweke wanihujumu, nabakia kulaani
Nilivyokuja narudi, sina la kujivunia
Kuondoka inabidi, kashindwa kuvumilia
Hizi zetu itikadi, sitaki kuaminia
Kukata tama si budi, kabisa nakosa nia