Yangu rununu hushiki, ujumbe sipati hata
Labda sijawafiki, usingehofu kusuta
Waona siwajibiki, kuelezwa sitakata
Hali sasa taharuki, mimi sitaki kujuta
Moyo wangu nilikupa, penzi lako nikazama
Nikakupenda kwa pupa, ukawa we kaditama
Kuchiti nikaogopa, mi sikutaka lawama
Tulivyokuwa ni bapa, kwako nishakata tama
Nishaacha kubigija, acha niwe bahaluli
Bahati yangu nangoja, atanipa tu Jalali
Leo hii najichuja, yangu tena usijali
Utapata wako koja, kuwa nawe ni ajali