Hali Gani Hii Ghali

by JackSwaleh , August 8, 2024

Moyo wangu wasumbuka, yaganda ya kwangu damu
Nafsi yasononeka, hali kwani yahujumu
Mwenzenu nadhoofika, maisha yanidhulumu
Hadi lini kufinyika, tayari nishagharimu

Adimu hizi mihela, majukumu yazidia
Hamuna hata cha kula, mate yanikaukia
Uko wapi ewe Mola, mwanao najifilia
Naziwacha hadi sala, sina pa kukimbilia

Sitachoka kujituma, bidii nitaongeza
Mabonde nayo milima, naamini nitaweza
Hatua nitazipima, jasho nalo kupanguza
Alivyonifunza mama, upole nitajikaza

Unaeza penda kusoma: "Ndoa Ndoano"