Baba wetu wa mbinguni, mbele zako nimerudi
Niko chini magotini, hali yangu inabidi
Kwa kukosoa imani, mema nikayakaidi
Nimepoteza ramani, pole kwa kubaidi
Yule mwovu kaninasa, kanipa vya ulimwengu
Kapiga zote anasa, kanifunga zake pingu
Sipatani na kanisa, nikaabudu miungu
Kwa wingi tu nikakosa, nirehemu ewe Mungu
Hivi nimejikubali, narejea kwako baba
Naomba unibadili, nitwae niliyobeba
Kwa hakika nilifeli, wa kujidunga hu mwiba
Niweke huru na kweli, kwenye ibada na toba